SIKU chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za
Mitaa Tawala za Mikoa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kusema kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amekopa kiasi cha sh bilioni
moja kwenye Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
(LAPF), Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Eliud Sanga, amekanusha.
LAPF pia imekana kuwasaidia fedha au vifaa Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi na Iringa Mjini, Peter Msigwa, kama ilivyosemwa bungeni.
Juzi, Ghasia alisema kuwa Mbowe anadaiwa sh bilioni moja na LAPF na
ametumiwa waraka wa kumkamata ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Waziri huyo alisema si kosa kwa wabunge kupewa fedha na LAPF, lakini ni kosa kwa mbunge kutorejesha fedha alizokopeshwa.
Kauli ya LAPF
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Sanga, alibainisha kuwa LAPF haijawahi
kumkopesha Mbowe sh bilioni moja, na kwamba mfuko huo hauna utaratibu
wa kukopesha mtu mmoja mmoja, hivyo hakuna mikopo ya aina hiyo.
“Mfuko wa LAPF hauna utaratibu wa kukopesha mtu mmoja, hivyo hakuna
mikopo ya aina hiyo na wanachofanya ni kutoa mikopo ya wanachama wake
kupitia vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na mikopo ya nyumba kwa
wanachama wanaokaribia kustaafu,” alieleza Sanga.
Alisema shughuli kuu za mfuko huo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, uwekezaji na kulipa mafao.
“Ieleweke kuwa ingawa waheshimiwa wabunge au mtu au taasisi yoyote
hazuiliwi kuomba msaada wa kijamii, Mbilinyi na Msigwa hawajawahi
kuwasilisha maombi na hawajawahi kupewa msaada wowote na LAPF.
Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari mbalimbali Mei 26 ambapo gazeti mojawapo lilikuwa na kichwa kilichosema ‘Waheshimiwa wabunge ni wasumbufu na kumfanya Mkurugenzi Mkuu asiende bungeni’ si za kweli,
alisema.
Alibainisha kuwa pamoja na majukumu hayo, mfuko unashiriki katika kuisaidia jamii kupunguza umasikini na kuchochea maendeleo.
Misaada hii ina lengo la kusaidia jamii yote ya Watanzania yenye mahitaji mbalimbali kwa kutambua kuwa misaada hii itawanufaisha si wanachama wa LAPF tu bali wananchi wote na kwamba imekuwa ikitoa misaada ya kijamii kwa wananchi wote.Imekuwa ikitoa misaada ya kijamii katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya afya, elimu, vituo vya watoto yatima, kusaidia mashuka, vyandarua na dawa kwa watu wanaokumbwa na maafa
alisema.
Aliongeza kuwa LAPF wamekuwa wakichangia elimu kwa kujenga madarasa, ununuzi wa madawati na vifaa vya maabara.
Hata hivyo, alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 LAPF
imetoa misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi katika
Chuo cha Madaktari Bugando na Chuo Kikuu Huria (OUT).
Alisema kuwa LAPF haizuii taasisi yoyote kuomba msaada wa kijamii kwa
kuwa hutoa misaada mbalimbali kwa kuzingatia mpango wa bajeti
iliyoidhinishwa kwa kuzingatia sera ya misaada ya kijamii na maombi
yaliyowasilishwa.
Sanga, alisema hata taasisi au mtu hapewi fedha mkononi taslimu, bali
LAPF inanunua vifaa na kuwasilisha moja kwa moja kwa wahusika.
0 comments:
Chapisha Maoni