Waziri Mkuu wa zamani wa Malaysia amesema Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA linaficha maelezo muhimu kuhusu hatima ya ndege ya Malaysia iliyotoweka. Katika taarifa aliyochapisha katika weblogu yake siku ya Jumapili, Mahathir Mohammad amesema CIA na shirika la utengenezaji ndege la Marekani, Boeing, kwa pamoja zinaficha maelezo kuhusu ndege iliyotoweka. Aidha amesema ni jambo la kushangaza kuona vyombo vikubwa vya habari duniani havifuatlii kwa kina kadhia ya ndege hiyo ya Malaysia. Mahathir amesema yamkini CIA iliongoza ndege hiyo kwa mbali na kuiweka katika mfumo wa kujiendesha yenyewe kisha ikatua eneo la siri na alama zake za Malaysian Airlines kuondolewa. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Malaysia iliyotoweka tarehe 8 mwezi wa Machi mwaka huu ikiwa na mamia ya abiria ilipokuwa inaelekea Beijing, China kutoka Kuala Lumpur Malaysia. Pamoja na kuwa nchi kadhaa zinashirikiana katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa lakini bado hakuna athari zozote za ndege hiyo ya kisasa aina ya Boeing 777-200ER iliyotengenezwa Marekani. Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak naye pia alinukuliwa akisema ndege ya abiria ya nchi hiyo iliyotoweka ilipotoshwa mkondo wake kwa makusudi na kuendelea kuruka angani masaa kadhaa hata baada ya kutoweka kwenye rada.
0 comments:
Chapisha Maoni