Jumanne, Aprili 22, 2014

WATU BINAFSI KUMILIKI TRENI NCHINI TANZANIA

Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajiwa kupata ushindani baada ya Serikali kuamua kuruhusu wawekezaji wa sekta binafsi kutumia Reli ya Kati.
Uamuzi huo wa Serikali huenda ukaongeza ufanisi kwa shirika hilo ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikumbwa na matatizo ya kiufanisi.
Baada ya kuanzishwa mwaka 2007, TRL ilikumbwa na misukosuko baada ya mwekezaji Rites kutoka India kushindwa kulisimamia kikamilifu na kusababisha hasara ya mabilioni. Kabla ya TRL reli ya kati ilikuwa chini ya Shirika la Reli (TRC) ambalo nalo halikuwa na ufanisi.
Akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya kuijengea uwezo TRL iliyofanyika Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka alisema kampuni binafsi zitaruhusiwa kuingiza treni zitakazotumia reli hiyo kwa kulipa ushuru kwa Serikali.
Kutokana na mabadiliko hayo, Dk Mwinjaka alisema Serikali imeanza kuiandaa TRL kupambana na ushindani utakaotolewa na kampuni hizo binafsi.
“Katika hii warsha tunawaandaa kujua kwamba utafikia wakati wanahitaji kujitegemea. Kwa misingi hiyo basi, tumepata wataalamu kutoka ndani na nje kuweka mawazo yao pamoja kujua ni namna gani mabadiliko hayo yatafanyika,” alisema Dk Mwinjaka.
Alipoulizwa kuwa uamuzi huo utaanza kutekelezwa lini, Mwinjaka alisema baada ya TRL kujengewa uwezo wa kuwa na mabehewa, injini na watumishi wa kutosha ili kuweka uwanja mzuri wa ushindani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRL, Severin Kaombwe alisema mpango huo huenda ukaanza baada ya mwaka 2015 kutoka na mkakati uliopo kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Kwa sasa tumeshaagiza vichwa (injini) 21 na takriban mabehewa 200 ambayo yanatarajiwa kufika ndani ya Agosti mwaka huu,” alisema Dk Mwinjaka huku akisisitiza kwamba mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa BRN.
Alisema injini na mabehewa hayo yana uwezo wa kurekebishwa kupita kwenye reli zote; za kawaida (ya kati) na ile ya kisasa inayotarajiwa kujengwa.
“Serikali imeamua kununua aina hiyo ya vifaa ili shughuli za usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kati ziendelee bila kuathiriwa wakati wa kujenga reli hiyo mpya na baada ya kukamilika tutarekebisha ili kupita njia mpya.”
Reli mpya ya kisasa inatarajiwa kugharimu takriban Dola za Marekani 6 bilioni (Sh9.6 trilioni) zinazofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

0 comments:

Chapisha Maoni