Jumatatu, Aprili 14, 2014

UCHUNGUZI UNAONESHA KUWA WANAFUNZI MASIKINI NDIO HUFELI ZAIDI

Watoto katika familia masikini ndio wanaoathirika kwa kiwango kikubwa kwa kushindwa kupata stadi za kuwawezesha kujua kusoma na kuandika wakiwa darasa la pili, ikilinganishwa na watoto waliopo katika familia tajiri.

Kwa mujibu wa utafiti uliotolewa katika uzinduzi wa ripoti maalumu ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) jana, Mratibu wa Asasi ya Uwezo Tanzania, Zaida Mgala alisema hiyo ni changamoto mpya kwa Serikali na watunga sera katika kukabiliana na tatizo la tabaka hilo linalozidi kukua.
Mgala alitoa takwimu hizo mbele ya aliyekuwa mgeni rasmi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa ambaye alisema Serikali inafarijika na utafiti huo ambao matokeo yake yatakuwa na msaada mkubwa katika uboreshaji wa sekta ya elimu.
Akisisitiza, Magala alisema: “Tumefanya utafiti wa moja kwa moja kwa kuwafuata watoto nyumbani na kuwafanyia majaribio. Tulilenga watoto wa darasa la pili tu kwa kuwa ndio wanaolengwa na silabasi, na tumebaini pengo kubwa. Zaidi ya asilimia 60 ya watoto kutoka familia zenye uwezo ndio waliofaulu. Watoto kutoka familia masikini walioweza kuonyesha upeo hawafiki asilimia 40.”
Alisema pamoja na tatizo hilo, walibaini kwamba asilimia 18 ya walimu 3,624 hawakuwepo kwenye vituo vyao vya kazi wakati wa utafiti huo, huku walimu watano kati ya 10 ndio walioingia darasani kwa muda unaotakiwa.
Alisema matatizo ya walimu ni suala la kupewa kipaumbele hasa kwa kuboresha mazingira yao ya kazi na masilahi, lakini walimu pia wanatakiwa kuwajibika ipasavyo kwa kufundisha kwa uadilifu na kwa moyo ili kusaidia kuinua uwezo na kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Alisema hali siyo nzuri hasa vijijini, ambapo walimu wengi wamekuwa wakifundisha saa mbili kwa siku badala ya saa tano kama inavyotakiwa.
“Tumebaini kwamba wakati mwingine kumbe hata serikali ikijitahidi kwa nguvu zake zote changamoto bado ni nyingi sana. Ni suala linalohitaji ushirikiano wa kutosha kutoka pande zote ili kuhakikisha tunafanikiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu nchini (TIE) ambayo ndiyo inayosimamia mitaala, Dk. Leonard Akwilapo alisema katika ujenzi wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa mwanafunzi anayeweza kufanya vyema ni lazima awe amehitimu kwa uhakika kufikia darasa la pili.
Alisema ni hakika kwamba mwanafunzi asipoweza kupata stadi hizo katika darasa la pili anaweza kuchukia shule, kuwa mtoro na kasha kuacha shule, kwa kuwa hataweza kwenda sambamba na mahitaji ya madarasa ya juu, yaani kuanzia darasa la tatu.
Dk Akwilapo alisema ubora wa mazingira ya kujifunzia pia ni tatizo, ambapo walimu wanatakiwa kuwa wenye stadi zinazostahili ili kuweza kutumia umahiri wao kuwafundisha wanafunzi kwa kiwango kinachokubalika, sio walimu ambao wamekuwa wakifundisha kwa mazoea.

0 comments:

Chapisha Maoni