Jumatano, Aprili 09, 2014

RAIS PIERRE NKURUNZIZA AKANA KUSAMBAZA SILAHA

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amekadhibisha vikali tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake kwamba anasambaza silaha kwa wananchi wa nchi hiyo. Rais Nkurunziza ameyasema hayo baada ya kukutana na Balozi wa Marekani mjini Bujumbura. Rais Nkurunziza amesisitiza kwamba zoezi la kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo halitafanyika. Naye Willy Nyamitwe Msemaji wa Rais Nkurunziza amesema kuwa, habari zilizoenezwa  kwamba Rais Nkurunziza anasambaza silaha kwa wananchi hazina ukweli wowote na zimetolewa kwa shabaha ya kuzichochea fikra za walio wengi nchini humo. Nyamitwe amesema kuwa Burundi itaitisha uchaguzi huru na wa haki kwa kutegemea katiba iliyopo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, tarehe 21 Machi, Bunge la Burundi  lilitupilia mbali mpango wa serikali wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni