Jumanne, Aprili 22, 2014

IVO MAPUNDA AAMUA KUACHANA NA TAULO LAKE

INAWEZA kuwa habari njema kwa timu zitakazocheza na Simba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara au mechi za kirafiki.
Kipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda amesema ataacha kulitumia taulo lake katika michezo atakayocheza ili kuwatoa wasiwasi mashabiki wa timu pinzani.
Tangu alipokuwa akiichezea Gor Mahia ya Kenya msimu uliopita, Mapunda amekuwa akitumia taulo ambalo hulitundika katika nyavu za goli analodaka ili kujifuta jasho mikono yake pindi inapoonekana kuwa inateleza kuokoa mashuti ya timu pinzani.
Hata hivyo, mashabiki wengi wamekuwa wakilihusisha taulo hilo na imani za kishirikina.
Taulo la Mapunda liliibua tafrani Jumamosi iliyopita katika mchezo wa Simba na Yanga uliochezwa Uwanja wa Taifa, baada ya dakika 56 Yanga kukosa bao la wazi huku kipa huyo akiwa ametoka langoni ambapo kila walipopiga mpira ulikuwa ukiwagonga mabeki wa Simba.
Ndipo Didier Kavumbagu akalifuata taulo hilo na kwenda kulirusha kwa mashabiki wa timu yake japokuwa halikuweza kuwafikia.
Mapunda ameiambia Fichuo Tz:
Nimeamua kuachana na taulo langu ili kuwatoa wasiwasi wapinzani wangu, unajua wengi wanadhani lina mambo ya uchawi sasa ili wacheze wakiwa huru na kujituma sitaingia nalo uwanjani badala yake nitabuni kitu kingine ambacho kitakuwa maarufu kama taulo.
Ninachofanya ni kuwapa burudani mashabiki wala hakuna kitu kingine cha ziada, lakini watu hawaelewi tazama Yanga walivyogombea taulo langu, mataulo yangu yote hayana uchawi wowote.

0 comments:

Chapisha Maoni