Jumatatu, Aprili 14, 2014

IDADI YA WALIOKUFA KATIKA MAFURIKO DAR ES SALAAM YAZIDI KUONGEZEKA, SASA NI WATU 13

Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko jijini Dar es Salaam imefikia watu 13 kufikia Jumatatu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka baada ya kupata taarifa za matukio ya mafuriko kutoka maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa siku tatu mfululizo tangu Ijumaa iliyopita, mvua kubwa ziliendelea kunyesha na kusababisha madhara makubwa vikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja, hivyo kukata mawasiliano na mikoa ya jirani ya Pwani na Morogoro na hata ndani ya mkoa wenyewe.
Karibu maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam yameathirika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko, huku wakaazi wa maeneo ya mabondeni wakiathirika zaidi baada ya nyumba zao kujaa maji.
Picha ya anga ya mafuriko jijini Dar es Salaam, Tanzania
Miundombinu ya barabara na madaraja mbalimbali yanayounganisha jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake pia imeharibiwa.
Mradi mwingine muhimu wa mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mafuriko hayo ambapo magari, mashine na mifuko ya saruji imechukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.
Shughuli za urejeshaji wa miundombinu zimekuwa zikiendelea ikiwa ni pamoja na matengenezo katika daraja la Mpiji linaloiunganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Hata hivyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania, TMA, yametahadharisha kuhusu kuendelea kunyesha kwa mvua na kuwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhama ili kusalimisha maisha na mali yao.

0 comments:

Chapisha Maoni