Bunge Maalumu la Katiba limeomba kuongezewa muda wa siku 60
kuanzia Agosti 5, mwaka huu litakapokutana kwa ngwe ya pili, Mwananchi
limebaini.
Bunge hilo linahitimisha ngwe yake ya kwanza
Aprili 25, mwaka huu likiwa limekutana kwa siku 67, kati ya 70
zilizokuwa zimetengwa awali.
Kwa muda huo wa ziada 60, iwapo wajumbe wote 629
watalipwa posho ya Sh300,000 iliyopangwa kwa siku, jumla ya Sh11.322
bilioni za walipakodi zitatumika ukilinganisha na Sh13.209 bilioni
zilizotumika katika siku 70 za awali. Jumla ya fedha zote zitakazotumika
kwa posho ni Sh24.53 bilioni, bila kuingiza gharama nyingine nje ya
posho za wajumbe.
Jana, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta
alitangaza kwamba shughuli za Bunge hilo zitakoma wakati wajumbe wake
watakapokwenda kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, Aprili
26, mwaka huu.
Sitta alisema jana kwamba aliwasilisha maombi ya kuongezewa muda kwa Rais Jakaya Kikwete, ambayo yalikuwa hayajajibiwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alipoulizwa
jana alisema: “Mheshimiwa Rais (Kikwete) anachoafiki ni kama ambavyo
kila mtu anaona mwenendo wa Bunge ulivyo, kwamba siku 70 haziwatoshi,
hivyo alikubali kwamba wanahitaji kuongezewa muda. Ingawa mpaka sasa
hajaamua atawaongezea siku ngapi, atakapoamua tutawafahamisha tu.”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema alisema upo uwezekano mkubwa wa Bunge hilo kuongezewa siku 60
lakini akaongeza kuwa hilo litategemea bajeti itakayoidhinishwa na
Serikali.
“Kwa kuwa kazi hii ndiyo kwanza iko katika hatua
zake za kwanza, ndiyo maana mchakato wake umesogezwa mbele mpaka Agosti
mwaka huu,” alisema Jaji Werema.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad
alisema: “Mwenyekiti hajanipa taarifa rasmi kwamba tutakutana kwa siku
ngapi, ila ninachofahamu ni kwamba tunasubiri barua rasmi kutoka kwa
Rais.”
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
nyongeza ya muda wa kukutana kwa Bunge hilo inatolewa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Hamad alisema tayari Sitta alishawasilisha maombi
ya kuongezewa siku za Bunge hilo kukutana, lakini akasema hana hakika
kama majibu tayari yamerejeshwa.
Hamad alisema wakati Bunge litakapoahirishwa litakuwa limebakiza siku tatu, ambazo zitafidiwa wakati watakapokutana Agosti 5.
Mmoja wa maofisa wa Bunge Maalumu alisema siku zilizoongezwa ni
60 na kwamba tayari yeye na maofisa wenzake walikuwa wanaandaa ratiba ya
siku hizo.
Katika siku ambazo Bunge hilo limekutana limefanya
kazi ya kuandaa na kupitisha kanuni za uendeshaji wake, kuchagua
viongozi wa Bunge Maalumu na kujadili sura mbili kati ya 17 za Rasimu ya
Katiba.
Katika hatua nyingine, Hamad alisema wanakusudia
kuifanyia marekebisho Kanuni ya 35 (6) ya Bunge hilo ili kuruhusu Kamati
ya Uandishi kufanya kazi ya majumuisho ya michango ya wabunge kuhusu
Ibara ya Kwanza na ya Sita ambazo zinaendelea kujadiliwa.
“Kwa mujibu wa Kanuni ya 35 (6), Kamati ya
Uandishi haiwezi kufanya kazi kabla ya Bunge kufanya uamuzi wake, sasa
tunataka kamati hiyo ifanye majumuisho yake kisha ilete mbele ya Bunge
ambalo litafanyia kazi majumuisho hayo,” alisema Hamad.
Alisema Kamati ya Uongozi ilielekeza Kamati ya
Kanuni ikutane ili kuandaa marekebisho ya kanuni hiyo ambayo
yatawasilishwa bungeni kufanyiwa uamuzi.
0 comments:
Chapisha Maoni