Watanzania 13 wametiwa mbaroni nchini Madagascar wakituhumiwa
kukutwa na meli iliyosheheni magogo ya miti adimu na ghali ambayo
yamepigwa marufuku kuvunwa humo.
Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), limesema
Watanzania hao wanashikiliwa tangu wiki iliyopita. AFP lilieleza kuwa
meli hiyo ambayo inadaiwa kusajiliwa Tanzania, ilikutwa ikiwa imesheheni
magogo hayo katika ufukwe wa Madagascar baada ya kupata hitilafu.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Usalama wa Jeshi la
Polisi Madagascar, Anthony Rakotoarison alikaririwa akisema meli hiyo
ilikutwa imebeba magogo 2,135 aina ya rosewood.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Tuki, Toleo la Tatu, rosewood ni mwaridi ikisema ni mti mwekundu na mgumu unaotumika kutengeneza samani.
“Ilikuwa ni meli ya Tanzania ambayo ilikuwa imepata hitilafu, tumeikamata,” alisema Rakotoarison.
Pakotoarison alisema walichunguza na kubaini
magogo hayo ya miti migumu yenye rangi nyekundu ambayo alisema
hayapatikani kwa wingi nchini humo hivyo kuilazimu serikali kupiga
marufuku uvunaji wake ili miti hiyo isiteketee.
Alisema miti hiyo ilipata heshima kubwa kimataifa na mahitaji yake yameongezeka kuanzia mwaka 2009.
Hivi karibuni, Rais wa Madagascar, Rais Hery Rajaonarimampianina alipiga marufuku biashara ya miti hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano
wa Kimataifa, Michael Haule alisema kuwa bado Serikali ya Tanzania
haijapata taarifa kuhusu kukamatwa kwa Watanzania hao pamoja na meli
yao.
“Bado sijapata taarifa hizo… Nitafuatilia na nitakujibu,” alisema Haule.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso
alisema ofisi yake inawasiliana na Polisi wa Kimataifa nchini (Interpol)
ili kupata undani wa habari hizo.




0 comments:
Chapisha Maoni