MDUNGUAJI wa watu takriban tisa wilaya ya Tarime mkoa wa mara,
alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi alipokuwa akipatiwa matibabu
katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime baada ya kuzidiwa na
vipigo vya Jeshi la Polisi, akigoma kutaja washirika wake.
Taarifa zilizotolewa na mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Roberty
Onesmo zilisema muuaji huyo, Charles Range Kichune (38) alifariki dunia
akiwa amelazwa katika wodi namba 8 Hospitalini hapo.
Onesmo alisema kuwa marehemu huyo ambaye mwili wake umehifadhi katika
chumba cha kuhifadhia maiti, alifariki muda mfupi majira ya saa 10.00
usiku wa kuamkia juzi, baada ya kufikishwa na askari Polisi.
Mhalifu huyo ambaye ni mkaazi wa kitongoji cha Ronga kijiji cha
Kenyamanyori kata ya Turwa wilaya ya Tarime, alikamatwa na askari Polisi
mkoani Tanga alikotorokea baada ya kufanya mauaji ya watu tisa na
kuwajeruhi wengine na kisha kuwapora vitu mabli mbali.
Jeshi la Polisi Tarime na Rorya na askari wa mkoa wa Tanga kwa
ushirikiano walifanikiwa kumkamata siku ya Februali 6, mwaka huu jioni
baada ya kukimbia wilayani hapa, alipojificha kwa muda kwa rafiki yake,
mhalifu Marwa Keryoba wa mtaa wa Nyabisare manispaa ya Musoma.
Katika upekuzi nyumbani kwa rafiki yake ambaye aliuawa na askari
polisi Februali 7 mwaka huu asubuhi katika mtaa huo, baada ya kukaidi
amri na kuwarushia risasi, kulikutwa silaha ya aina ya SMG iliyokatwa
kitako na mtutu ambayo Charles Range Kichune maarufu ‘’KENONKE’ alikiri
kuitumia katika matukio ya mauaji na unyan’ganyi kwa wananchi 9.
Muuaji huyo alikiri kuifunga tochi silaha hiyo iliyotumika kumulika
wakati wa kuendesha matukio hayo ambapo miongoni mwa watu waliouawa ni
pamoja na mstaafu wa Jeshi la wananchi (Jwtz) na komando ambaye ni mtoto
wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa (Wabachira).
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya Justus Kamugisha alithibitisha
kukamatwa kwa muuaji huyo mkoani Tanga, na silaha hiyo ya kivita pamoja
na simu na vitu mbali mbali alivyovipora kwa watu waliouawa na
kujeruhiwa katika vijiji vya Mogabiri, mjini Tarime, Nkende ,Rebu na
Nyamwaga.
Aidha kamanda Kamugisha alithibitisha kufariki dunia muuaji huyo
katika Hospitali hiyo baada ya kupelekwa kupatiwa matibabu na kwamba
Jeshi la Polisi Tarime na Rorya linaendelea kuwasaka wahalifu wengine.




0 comments:
Chapisha Maoni