Serikali inapoteza Shilingi trilioni 1.6 kila mwaka kutokana na
kuzalisha umeme wa mafuta mazito. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini, Victor Mwambalasa, aliyasema hayo jana jijini Dar es
Salaam, wakati kamati ilipotembelea bandarini ya Dar es Salaam.
Wajumbe wa kamati hiyo walishuhudia shehena ya mwisho ya mabomba
269 ya mradi wa bomba la gesi yaliyoagizwa kutoka China ikisafirishwa
kwenda Mtwara.
Alisema miundombinu ya bomba hilo ikikamilika itaokoa Sh
trilioni 1.6 zinazopotea kila mwaka kutokana na mitambo inayotumia
mafuta mazito kufua umeme.
Aliongeza kuwa, hivi sasa zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa
nchini unatokana na gesi asilia na kwamba kwa muda mrefu serikali
iliazimia kutumia nishati hiyo kufidia pengo la mahitaji ya umeme
kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na ukame, unaokwamisha umeme wa
maji.
Mabomba hayo yalikuwa yakipakuliwa kutoka katika meli ya China
yenye urefu wa mita 180 na kuingizwa kwenye malori yanayoyapeleka
Mtwara.
Mwambalasa amewaomba wadau kuwa wajumbe wa kuelimisha wananchi wenye lengo la kupotosha ukweli kuhusu mradi huo.
“Ikumbukwe kuwa lengo la serikali ni kuboresha maisha ya wananchi kwa kupunguza umaskini,” alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliachim Maswi, alisema mradi huo utakapokamilika, tatizo la umeme
litamalizika na kubakia historia.
"Ndiyo maana leo kamati yenu imekuja bandarini kushuhudia hili,
lakini pia zipo ziara mbalimbali zinazofanywa kule Mtwara na mwezi ujao
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal atakwenda," alisema.
Alisema kilometa 499 za mkuza wa bomba (njia) zimekamilika ikiwa ni asilimia 99 ya kazi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TDPC), Yona
Killagane, akielezea kuhusu ujenzi wa bomba hilo alisema umekamilika
kwa asilimia 45.
Alisema usimikaji wa mitambo unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Desemba na majaribio ya mitambo yatafanyika mwezi huo.
Alisema tayari zaidi ya kilometa 280 za mabomba yameshapangwa kwenye mkuza.
Kuhusu uwekaji wa mabomba kwenye njia yake na kuweka mkongo wa
mawasiliano sambamba na bomba alisema kilometa zaidi ya 90 zimekamilika.
Alisema ujenzi wa bomba hilo unaotarajiwa kukamilika Mei mwakani
ulianza mwezi uliopita na kwamba hadi sasa zaidi ya kilometa nne
zimekamilishwa.




0 comments:
Chapisha Maoni