Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen atalikamua
Shirikisho la Soka nchini (TFF), Sh. milioni 420 endapo likifikia uamuzi
wa kuachana naye kabla ya mkataba wake kumalizika Mei mwakani.
Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi alisema jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki kuwa hatma ya kocha huyo itajulikana Februari 24,
mwaka huu (Jumatatu ijayo).
“Kwa sasa siwezi kueleza chochote kuhusu Poulsen kwa sababu si wakati
mwafaka wa kuzungumzia suala hilo. Februari 24, mwaka huu kila kitu
kitafahamika, tuombe uzima tu,” alisema Malinzi huku taarifa kutoka
ndani ya shirikisho hilo zikidai kuwa wamejipanga kumtupia virago raia
huyo wa Denmark ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha kikosi cha
Taifa Stars.
Alipotafutwa na NIPASHE jijini mwishoni mwa wiki, Poulsen alisema
hajali kinachozungumzwa kuhusu kuvunjwa ama kutovunjwa kwa mkataba wake.
“Ninachojali ni kazi yangu, natekeleza majukumu yangu kama kocha wa timu ya taifa bila kujali yanayozungumzwa,” alisema Poulsen.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha
Mapato ya TFF iliyotolewa Mei 2011, kocha wa Taifa Stars analipwa
mshahara wa Sh. milioni 315 kwa mwaka (Sh. milioni 26.25 kwa mwezi),
kama TFF ikisitisha mkataba wa Poulsen, italazimika kumlipa Sh. milioni
420 ambazo ni mshahara wake wa miezi 16 iliyobaki kuanzia mwezi huu
kabla ya kumalizika kwa mkataba wake Mei mwakani.
Ukurasa wa tano wa kiambatanisho cha 7(A) cha ripoti hiyo yenye jumla
ya kurasa 95 na viambatanisho tisa unafafanua kuwa jumla za gharama za
kocha wa Taifa Stars kwa mwaka ni Sh. milioni 416 ikiwa ni mshahara,
nyumba (Sh. milioni 45), usafiri wa kwenda kwao na kurudi (Sh. milioni
20.4), usafiri wa ndani (Sh. milioni 33.6) na bima ya afya (Sh. milioni
mbili.
Pengine gharama hizi kubwa ndizo zinazousukuma uongozi mpya wa TFF,
ambao umeshaeleza kuvutiwa na makocha wazawa, kufikiria kumtema kocha
huyo wa zamani wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 18
(U-18) ya Singapore.
Lakini mshahara wa Poulsen unalipwa na Serikali ya Tanzania kupitia
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo baada ya Rais Jakaya
Kikwete kuagiza mishahara yote ya makocha wa timu za taifa ilipwe na
serikali.
Watendaji wa wizara yenye dhamana ya michezo nchini hawakupatikana
jana kuzungumzia suala hilo endapo serikali itakuwa tayari kulipa
gharama hizo au mzigo huo utabaki kwa TFF.
Poulsen, aliyekuwa akizinoa timu za taifa za vijana, alisaini mkataba
wa mwaka mmoja Mei 11, mwaka juzi kuinoa Stars akirithi mikoba ya kocha
Jan Poulsen ambaye pia ni raia wa Denmark, mkataba uliomalizika Mei 15,
mwaka jana kabla ya kusaini tena mpya wa miaka miwili ambao utamalizika
Mei mwakani.
Wakati Malinzi akisita kueleza hatma ya Poulsen, tayari shirikisho
hilo limeshaamua kuwatumia makocha wazawa katika mkakati wake wa kupata
kikosi imara cha Stars kupitia michuano rasmi ya kitaifa itakayoanza
Februari 22 hadi Machi 5, mwaka huu. Mikakati hii inafanywa bila
kumshirikisha.
Kwa muda mrefu sasa baadhi ya wadau wa soka nchini wamekuwa wakiponda
kiwango cha Stars, hasa katika kampeni za Kombe la Dunia zitakazopigwa
nchini Brazil kuanzia Juni 12 hadi Julai 13.
Stars wakiwa katika Kundi C, Septemba mwaka jana waliishia hatua ya
makundi baada ya kufanya vibaya katika mechi za marudiano na kumaliza
nafasi ya tatu; nyuma ya Ivory Coast na Morocco huku Gambia wakiwa
nafasi ya nne.



0 comments:
Chapisha Maoni