Alhamisi, Januari 02, 2014

UCHAMBUZI WA CNN JUU MAZUNGUMZO YA NYUKLIA IRAN 2013

Kanali ya televisheni ya CNN imeuelezea mwaka 2013 kuwa ni mwaka uliokuwa na mafanikio nadra kuwahi kushuhudiwa katika kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa mujibu wa kanali hiyo, katika mwaka uliomalizika wa 2013 limetokea tukio katika uga wa kimataifa ambalo ni tofauti kabisa na mazungumzo yote yaliyofanywa hapo kabla kati ya Iran na jamii ya kimataifa, na kupatikana matunda katika mazungumzo hayo. Kinachoashiriwa na CNN ni makubaliano ya Novemba 24 baina ya Iran na nchi sita zinazojulikana kama kundi la 5+1, ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia na Ujerumani; makubaliano ambayo yalifikiwa huko Geneva baada ya takribani miaka kumi ya misuguano na propaganda dhidi ya shughuli za nyuklia za Iran. Kwa mtazamo fulani, makubaliano hayo ni azimio la kisiasa la mpango wa pamoja wa pande mbili unaokusudiwa kutekelezwa kwa sura ya kujitolea ili kujenga hali ya kuaminiana katika kadhia ya nyuklia na hatimaye kufikia kwenye lengo la pamoja.

Kwa mtazamo mwengine tunaweza pengine kusema kuwa katika kipindi kipya cha urais hapa nchini yameshuhudiwa mabadiliko maalumu ambayo natija yake ni makubaliano ya awali yaliyofikiwa Novemba 24 huko Geneva. Bila ya shaka mabadiliko hayo yametokana na majimui ya tajiriba na matukio yaliyojiri katika mazungumzo ya nyuklia ambayo yameyafanya madola ya Magharibi yachukue msimamo unaozingatia uhalisia wa mambo kutokana na hatua za Iran za kujenga hali ya kuaminiana katika suala la nyuklia. Hata hivyo msimamo huo umechukuliwa kwa kuchelewa kwa muda wa miaka kadhaa, kwa sababu viongozi wa juu kabisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikwishatangaza mara kadha wa kadha kwamba taifa hili halina nia ya kumiliki silaha za atomiki na kwamba kutokana na imani, itikadi na thamani za kidini, silaha hizo hazina nafasi yoyote katika mfumo wake wa ulinzi. Kinyume na vile unavyojaribu kuonyesha ulimwengu wa Magharibi, sera za msingi na za utekelezaji za Iran zinasisitiza juu ya kutekelezwa kikamilifu mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT. Na kwa kweli makubaliano ya Iran na kundi la 5+1 katika kadhia ya nyuklia yamefuata muelekeo huo. Na ndiyo maana licha ya kupokewa na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa, makubaliano hayo yameuchukiza mrengo maalumu unaojumuisha utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekuwa ukificha ukweli kuhusu silaha zake za atomiki nyuma ya pazia la zogo na propaganda dhidi ya shughuli za amani za nyuklia za Iran. Katika kipindi chote cha miaka ya hivi karibuni, Israel, ambayo ni mmiliki pekee wa silaha hatari za atomiki katika Mashariki ya Kati imekuwa ikitumia kila fursa inayopata ikiwemo ya vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujaribu kuuhadaa ulimwengu kwa kutoa taswira potofu na ya kupindua ukweli kuhusu shughuli za nyuklia za Iran. Nukta nyengine kuhusu sababu zilizochangia kupatikana mwafaka kati ya Iran na kundi la 5+1 ni kugonga mwamba madola ya Magharibi katika sera yao ya kuiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu na visivyo na uhalali wa kisheria. Kutokana na tajiriba yaliyopata, madola hayo yametambua kwamba taifa la Iran halitosalimu amri kwa sababu ya vikwazo, wala halitoyumbishwa na vitisho vya Magharibi. Isitoshe ni kwamba zile nchi ambazo kwa muda wote huu zimekuwa zikifuata mkumbo katika sera ya vikwazo inayotekelezwa na Marekani hazina hamu tena ya kushabikia suala hilo linalozigharimu na kuzipotezea mabilioni ya dola. Lakini nukta ya mwisho ni kwamba makubaliano ya Geneva yalikuwa ushindi kwa wote na yalithibitisha kuwa, kwa kufikia makubaliano ya pamoja na kwa kuheshimiana, inawezekana kufikia kwenye ufumbuzi wa kimantiki. Pamoja na yote hayo makubaliano ya Geneva ni hatua ya kwanza mbele kuelekea kwenye mwafaka kamili. Hatua hiyo ilipigwa katika mwaka 2013, na ilivyokubaliwa, mnamo mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, itaanza awamu ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Ndiyo kusema kwamba bado kuna safari ndefu na ngumu hadi kufikia kwenye mwafaka kamili

0 comments:

Chapisha Maoni