Alhamisi, Januari 09, 2014

MKE WA RAIS WA KWANZA WA ZANZIBAR, MAMA KARUME AITETEA YANGA

Mdhamini wa klabu ya Yanga, Mama Fatuma Karume amesema Yanga hawajakurupuka kukacha michuano ya Mapinduzi ila wana sababu zao za msingi na ndiyo maana wamefanya hivyo.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Mahisara jana, Mama Karume alisema Yanga siyo wajinga kuamua kujitoa kwenye michuano hiyo, ambapo badala ya watu kuwalaumu walitakiwa waulize sababu za Yanga kujitoa.
“Yanga hawajakataa Mapinduzi, Mapinduzi ni ya Serikali, nina hakika kabisa Yanga hawajakataa haya Mapinduzi, walichokikataa ni michezo ya mapinduzi, na wana sababu zao, hao waandaaji wameona Yanga wamejitoa mara tatu mfululizo kwa nini wasiwatafute Yanga wakakaa chini na kuyamaliza?”alihoji Mama Karume.
Alisema, “Hata siku moja waandaaji wa michuano ya mapinduzi hawajawahi kunifuata hapa wakaniambia habari za Yanga na hapa wanapajua viongozi chungu mbovu wa michezo wa Dar na Zanzibar wananifahamu, wangekuja kwangu mimi lazima ningewaita Yanga niwaulize kulikoni, lakini wao hawajafanya hivyo.”
Mama Karume alisema, “Najua kama Yanga wamejitoa na mwaka jana walileta watoto waandaaji wakawafukuza, sasa wangenifuata tukakaa na Yanga tukazungumza, Yanga si wajinga eti kujitoa, kwani mtu hakatai kunywa maji kama hayamdhuru, ukiona kakataa basi jua yanamdhuru.”
“Wao mwaka wa kwanza wamejitoa, wakapiga makelele kwenye vyombo vya habari ikapita, mwaka wa pili wamejitoa, mwaka wa tatu wameleta vitoto mkawafukuza, hamjiulizi tu kuna kitu gani mkakaa chini kuzungumza?”alihoji Mama Karume.

0 comments:

Chapisha Maoni