Ijumaa, Januari 24, 2014

MADEREVA WA BODA BODA 870 WAMEFARIKI DUNIA NA WENGINE 5,237 KUJERUHIWA VIBAYA KATIKA AJALI

Waendesha pikipiki 870 wamepoteza maisha na wengine 5,237 wamejeruhiwa katika matukio tofauti ya ajali za barabarani zilizotokea mwaka jana.
Hata hivyo, tathmini inaonyesha matukio ya ajali za pikipiki kwa mwaka huo ni 6,831 ambazo zilisababisha jumla ya vifo 1,098 wakiwemo waendeshaji hao.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani nchini, Mohamed Mpinga katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari hivi karibuni alibainisha kwamba idadi hiyo ya vifo imesababisha ongezeko la matukio hayo kwa asilimia 18.5 ikilinganishwa na matukio 5763 yaliyotokea mwaka juzi.
Alisema pia wapanda baiskeli 447 nao wamekufa katika kipindi hicho na 1,162 walijeruhiwa, wakati madereva 297 walikufa na wengine 1,528 walijeruhiwa kwenye ajali hizo.
“Wasukuma mikokoteni waliokufa mwaka jana ni 36 wakati 156 walijeruhiwa, kwa upande wa waendao kwa miguu 1,248 walipoteza maisha na wengine 836 walipata majeraha, pia upande wa abiria 1,105 walikufa huku 8,770 wakijeruhiwa, “ alisema Kamanda Mpinga katika taarifa yake hiyo.
Alifafanua kwamba mwaka jana kulikuwa na ongezeko la matukio ya ajali 264 katika jumla ya matukio 23,842 ikilinganishwa na ajali 23,578 zilizotokea mwaka juzi (2012).
Alisema ajali hizo zilizosababisha vifo ni 3,427 ikiwa ni ongezeko la matukio 99 sawa na asilimia 3.0 ya ajali zilizotokea mwaka 2012.
Pia aliitaja mikoa iliyoongoza kwa ajali, ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matukio ya ajali 12,983 ikifuatiwa na Kilimanjaro ajali 1,599 na Pwani ajali 1,460.

0 comments:

Chapisha Maoni