Ijumaa, Januari 24, 2014

JOHN MNYIKA AMPIGA JIWE PINDA

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwajibika kwa madai ya kushindwa kudhibiti ujangili wa tembo unaofanywa katika pori la Ugara lililopo kwenye hifadhi ya taifa jimboni mwake.
Mnyika alitoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye mkutano uliofanywa na chama hicho jana katika Kijiji cha Inyonga, Jimbo la Mpanda Mashariki katika mikutano ya Operesheni ‘Pamoja Daima’ na kudai kwamba, pori hilo ni miongoni mwa yaliyokithiri na kuongoza kwa ujangiri nchini.
Alidai kuwa, jimbo hilo la Pinda ni miongoni mwa majimbo maskini uliosababishwa na uzembe wa Pinda mwenyewe kushindwa kutumia rasilimali zilizopo jimboni humo ili kuliletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema kuwa, Pinda anakazana kuimba nyimbo na kushikilia ndoto zake za ufugaji nyuki huku wananchi wake wakiendelea kusota na umaskini.
“Poleni sana wananchi wa Mpanda, ninawaonea huruma sana kwani mnakumbana na hali hii ya umaskini kwa sababu ya kiongozi wenu Pinda. Hamuwezi kuondokana na umaskini kwasababu kiongozi wenu haonyeshi dalili za kuondokana na umaskini,” alisema Lema.
Waliokuwamo katika msafara huo jimboni humo ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Zanzibar, Said Issa Mohamed, Mnyika, na Lema.

0 comments:

Chapisha Maoni