Seleman Rajab (17) anaugua ugonjwa ambao mpaka sasa wazazi wake
wanasema hawaufahamu. Licha ya kuwa na maumivu na uvimbe kuongezeka,
mara ya mwisho kupelekwa hospitali ilikuwa mwaka 2010, zaidi amekuwa
akipewa vidonge vya kutuliza maumivu.
Mama yake anayemlea Khadija Ahmed anasimulia kuwa, alielezwa kwamba Rajab alizaliwa akiwa na uvimbe kwenye unyayo.
Akiwa na umri wa miaka miwili hakuweza kutembea,
akapelekwa hospitali kufanyishwa mazoezi ya viungo na alipotimiza umri
wa miaka sita, uvimbe huo ukaanza kututumka kidogo kidogo.
“Alikuwa akiishi na mama yake ambaye alifariki
Agosti mwaka jana, hakutuambia hospitalini aliambiwa mtoto anaugua nini,
lakini mara ya mwisho kumpeleka hospitali ya CCBRT ilikuwa mwaka 2010
na kwa sababu ilipendekezwa akatwe mguu, mama yake hakumrejesha tena,”
mama Seleman
Anasema tangu waanze kuishi na mtoto huyo, mwaka
jana hawajampeleka hospitali yoyote kutokana na kukosa fedha ya
kugharamia vitu mbalimbali ikiwamo kukodi gari la kumpeleka hospitali na
kumrejesha nyumbani.
Baba Selemani anafanya kazi ya kutunza bustani
kwenye kiwanda cha Kamal Steel, kinachotengeneza nondo na mama yake ni
mama wa nyumbani ambapo familia yake ni yenye watoto watano, wa kike
mmoja wa kiume. Wadogo zake wanasoma shule.
Selemani anasema, “Naomba nisaidiwe angalau na
mimi niwe na uwezo wa kutoka nje au kujihudumia mwenyewe badala ya sasa
ambapo ninaogeshwa, nikitaka kutoka nje mpaka baba na mama waniweke
kwenye blanketi, wanibebe mmoja huku mwingine kule, inaniuma sana.”
Anasema huwa anapata maumivu mara moja, kwamba
huhisi viungo hususan mguu uliovimba kama vile ndani yake kuna moto
unawaka na kwamba inapotokea hali hiyo, hupewa vidonge vya kutuliza
maumivu; mara nyingi humsaidia kupunguza maumivu.
Tangu mwaka jana, mguu wa kushoto nao umeanza
kuvimba. Hata sikio linaonekana kuanza kuvimba. Pamoja na matatizo yote
yanayomkabili tangu utoto, Seleman anaweza kusoma na kuandika majina
yake na ya wazazi wake.
Anasema alikuwa akifundishwa na marehemu mama
yake, kwamba alinunua ubao mdogo ambao alikuwa akiutumia kumfundishia
kusoma na kuandika.
Hakuwahi kuingia darasani na anasema ikitokea Mungu akamponya, atasoma sana ili awe mwalimu au daktari.
0 comments:
Chapisha Maoni