Jumatano, Septemba 11, 2013

HIKI NDICHO KIMEMUUA MSANII WA BONGO MOVIE MALISA

TASNIA ya filamu Bongo imepata pigo lingine baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuondokewa na msanii aliyekuwa akichipukia kwa kasi aliyefahamika kwa jina la Zuhura Maftah ‘Malisa’.
Malisa alifariki dunia katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar baada ya kusumbuliwa na uvimbe kichwani kwa takriban miezi mitatu.
Wakizungumza na gazeti hili mara baada ya kifo hicho, baadhi ya wasanii wa filamu walielezea masikitiko yao na kusema hakika wamemkosa msanii ambaye siku za baadaye angekuwa moto wa kuotea mbali.
“Kifo chake kimetusikitisha sana, Malisa alikuwa mmoja wa wasanii ambao walikuwa wakija kwa kasi, amefariki dunia wakati ndiyo kwanza nyota yake ilikuwa imeanza kung’ara lakini kazi ya Mungu siku zote haina makosa, akapumzike kwa amani,” alisema mmoja wasanii aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Msanii mwingine wa filamu ambaye huenda kifo hicho kimemgusa kuliko wengine ni Yvonne Cheryl ‘Monalisa’ ambaye inadaiwa muda mfupi kabla ya Malisa kufariki waliongea na kumwambia anaendelea vizuri.
Mmoja wa watu waliokuwa wakimhudumia Malisa hospitalini hapo aliyefahamika kwa jina la Vanitha alisema: “Siku ya kifo chake aliniambia nimpigie simu Mona aongee naye kwani hajamuona siku hiyo, ilikuwa saa 12 jioni baada ya kumaliza kumuogesha.
“Waliongea na kumwambia anaendelea vizuri. Baada ya Malisa kumaliza kuongea na Mona niliondoka lakini nilipofika Surender Bridge nikapata taarifa kuwa amefariki dunia,” alisema Vanitha.

0 comments:

Chapisha Maoni