Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP)Augustine Mrema
amejitetea akisema si kibaraka au pandikizi la CCM baada ya kukataa
kuungana na wapinzani wenzake kususia mjadala wa Sheria ya Marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 jana na juzi.
Akichangia mjadala huo, Mrema ambaye ni Mbunge wa
Vunjo, alisema hakutoka nje kwa kuwa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya
Demokrasia Tanzania (TCD) inayoundwa na vyama vyote vya siasa vyenye
wabunge kikiwamo CCM.
Huku akishangiliwa na wabunge wa CCM, Mrema
alijigamba kuwa yeye ni bosi wa vyama vyote ndiyo maana ilibidi abaki
bungeni ili kuangalia kinachoendelea. Alisema kama angeamua kutoka kama
walivyofanya wabunge wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, basi ingekuwa sawa
na kushindwa kusimamia majukumu yake ya TCD kikamilifu.
Mrema alikuwa akichangia hoja hiyo wakati wabunge vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi wakiwa wametoka.
Juzi usiku, Mrema alikuwa mbunge pekee wa upande
wa upinzani aliyebaki ndani ya Ukumbi wa Bunge baada ya wabunge wengine
kutoka wakipinga kujadiliwa kwa muswada huo bila ya kuwashirikisha
kikamilifu wadau wa siasa kutoka Zanzibar.
0 comments:
Chapisha Maoni