Polisi nchini Indonesia wamesema
mmoja wa wahubiri wa Kiislamu wenye msimamo mkali nchini humo ni
mshukiwa katika kisa cha usambazaji wa ujumbe na picha chafu za ngono.
Rizieq
Shihab anatuhumiwa kutuma ujumbe wenye maneno mazito ya mahaba na pia
picha za utupu alipokuwa anawasiliana na mwanamke mmoja.
Mhubiri huyo, ambaye kwa sasa yupo nchini Saudi Arabia, amekanusha madai hayo.
Bw
Rizieq ni kiongozi wa kundi la Islamic Defenders Front (FPI), ambalo
liliongoza maandamano makubwa dhidi ya gavana wa zamani wa mji mkuu wa
Jakarta Basuki Tjahaja Purnama ambaye alifungwa jela kwa kosa la kuitusi
dini ya Kiislamu mwezi uliopita.
Mhubiri huyo ambaye anafahamika
sana kwa hotuba na mahubiri yake yenye ujumbe wenye kuzua utata, tayari
amefungwa jela mara mbili awali kwa kuzua fujo na kuvuruga amani.
Katika
kisa cha sasa, Bw Rizieq anadaiwa kukiuka sheria kali za kukabiliana na
uenezaji wa ujumbe, picha au video chafu kwa kutuma ujumbe na picha kwa
mwanaharakati Firza Husein, ambaye pia ametajwa kama mshukiwa.
0 comments:
Chapisha Maoni