Aliyekuwa waziri wa habari,
utamaduni, Sanaa na michezo nchini Tanzania Nape Nnauye amesema bado
anaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kujaribu kufanikisha
mageuzi nchini humo.
Bw Nnauye, akizungumza wakati wa kukabidhi
rasmi afisi kwa mrithi wake Dkt Harrison Mwakyembe, kadhalika amesema
ataendelea kushirikiana na wizara hiyo.
Amesema yeye ni mdau mkubwa katika sekta zilizomo chini ya wizara hiyo.
Bw
Nnauye alifutwa kazi wiki iliyopita siku moja baada yake kupokea ripoti
ya kamati ya uchunguzi kuhusu uvamizi uliotekelezwa na mtu anayedaiwa
kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika studio za kituo
cha habari cha kibinafsi cha Clouds.
Kamati hiyo, kwenye ripoti yake, ilionekana kumkosoa Bw Makonda na kusema alitumia vibaya mamlaka yake.
"Heshima
aliyonipa mheshimiwa Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumuunga mkono
katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini," alisema Bw Nnauye,
kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya habari na michezo Tanzania.
Taarifa hiyo inasema Bw Nnauye ameahidi ataendelea kuwa mtiifu kwa Rais Magufuli, serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Bw Nnauye, ambaye ni mbunge wa Mtama, alisimamia wizara hiyo kwa miezi 15.
Waziri mpya Dkt Mwakyembe amesema anategemea kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa Bw Nnauye.
0 comments:
Chapisha Maoni