Jumapili, Januari 17, 2016

SULEIMAN MATOLA MPIGA DONGO KERR BAADA YA KUONDOLEWA SIMBA

Kocha msaidizi wa zamani wa Simba, Suleiman Matola, amesema Simba imechelewa kumtimua Kocha Dylan Kerr kwani alianza muda mrefu kutibua mambo.
Hivi karibuni Matola aliamua kuondoka mwenyewe Simba na kujiunga na Geita Gold Sports ya Ligi Daraja la Kwanza kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoelewana kwake na Kerr ambaye ni raia wa Uingereza.
Simba mapema wiki hii ilitangaza rasmi kuvunja mkataba na Kerr kwa kilichoelezwa kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika mechi zake za michuano mbalimbali.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Matola alisema: “Kerr ni kocha mzuri ila nilishawaambia viongozi mapema kuwa hafai ndani ya timu kutokana na yeye kutaka kufuata kile anachokiamini bila ya kushirikiana na wenzake hata kama anakosea.
“Simba imechelewa kumtimua kwani ameiweka timu mahali pabaya na kama angeondoka mapema usikute klabu ingekuwa pazuri sasa,” alisema Matola.
Wakati huohuo, Simba ambayo pia imemtimu kocha wake wa makipa, Idd Salim, hadi jana jioni ilikuwa ikiendelea na mazungumzo na Hemed Morocco ili achukue nafasi ya Kerr. Salim aliondoka jana usiku kurudi kwao Kenya baada ya kulipwa haki zake lakini Kerr bado yupo jijini Dar es Salaam akisubiri kulipwa haki zake.

0 comments:

Chapisha Maoni