WIZARA ya Ujenzi imeinyang’anya Kampuni ya Agriculture and Animal
Food Industries Ltd (Saafi), inayomilikiwa na mwekezaji mzalendo na
mwanasiasa mkongwe, Dk. Chrisant Mzindakaya nyumba 12 za umma ambazo
ilikuwa imezipanga kibiashara kwa miaka 12.
Nyumba hizo 11 za kuishi na moja ofisi zilizojengwa na Shirika la
Maendeleo la Norway mwaka 1988, zimekabidhiwa rasmi Juni 17 mwaka huu,
kwa Wakala wa Majengo (TBA), mkoani hapa na Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo wa serikali
baada ya kukagua nyumba hizo juzi, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi
Hilaly (CCM), alisema ana furaha kwani nyumba hizo zilikuwa zikimnyima
usingizi kutokana na maofisa serikalini wakiwemo majaji na baadhi ya
wakuu wa idara kuishi nyumba za kupanga, lakini sasa wataishi nyumba
hizo ambazo ni bora na zenye usalama wa kutosha.
Alibainisha kuwa baada ya kutembelea nyumba hizo na kuzikagua
akiongozana na Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Rukwa, Deocles
Kalikawe, amebaini kuwepo kwa upungufu mkubwa ambao alidai mwekezaji
aliyezipanga kibiashara atalipia gharama zote za ukarabati.
0 comments:
Chapisha Maoni