Vitendo vya baadhi ya wazazi, kudhalilisha walimu vinaendelea, ambapo
mzazi mmoja Selemani Juma, amewashambulia walimu wawili kwa viboko.
Amefanya hivyo kupinga mwanawe kurudishwa nyumbani, akashone kaptura. Alifanya hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa zilizotufikia zilibainisha kuwa Juma alidhalilisha
walimu wawili wa Shule ya Msingi Nzogimlole iliyopo wilayani Nzega
mkoani Tabora. Aliwashambulia kwa viboko, akipinga kitendo cha mwalimu
mmojawapo, kumrudisha nyumbani mwanawe.
Tulifika katika shule hiyo, yenye walimu tisa tu na
kuzungumza na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel Josephat, ambaye alisema
mwanafunzi huyo, Shaaban Maziku anayesoma darasa la pili, alipeleka
ujumbe tofauti na alioagizwa na walimu kwa baba yake, hivyo kusababisha
kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Josephat, mwalimu aliyedhalilishwa (jina
limehifadhiwa), alikuwa akifundisha katika darasa hilo na alipomuona
mwanafunzi huyo kavaa kaptura iliyochanika vibaya, kiasi cha sehemu za
siri kuonekana, alimrudisha nyumbani kwenda kurekebisha sare yake.
Mwalimu Josephat alisema mwalimu huyo wa kiume wa darasa la pili,
alimwagiza mwanafunzi wake aende kwa baba yake, akamuombe amsaidie
kushona kaptura hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni