Serikali ya Rwanda imesema hatua ya kuwatimua maafisa
sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia
uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa
kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.
Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa
kimataifa ,Bi Louise Mushikiwabo, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter
ameeleza kwamba Rwanda ilikuwa na haki zote kuwafukuza mabalozi wa
Afrika Kusini mjini Kigali ikizingatia hatua ambayo nchi hiyo ilianzisha
yenyewe kwa kuwatimua maafisa wa ubalozi wa Rwanda mjini Johannesburg.
Katika ujumbe wake mfupi kwenye
mtandao huo Bi Mushikiwabo, anailaumu Serikali ya Afrika Kusini kwa
kutochukua hatua dhidi ya wanyarwanda waliokimbilia nchini humo ambao
serikali ya Rwanda inawatuhumu kuendelea na hujuma za kigaidi dhidi ya
Rwanda na kwamba Pretoria haijatekeleza muafaka uliofikiwa awali.
Kulingana na kiongozi huyo kupitia mtandao wa
twitter, mahusiano mema kati ya Rwanda na Afrika Kusini yatafikiwa
wakati suala la kisheria kuhusu wanyarwanda waliokimbilia nchini humo
itapata ufumbuzi.
Wakati haya yakiarifiwa ,mjumbe maalum wa Rais
Baracka Obama wa Marekani katika mataifa ya ukanda wa maziwa makuu, Russ
Feingold,alisema kuwa Marekani inafuatilia kwa karibu mzozo huo ambao
alielezea waandishi kwamba mataifa ya Rwanda na Afrika ya kusini hayana
budi kumaliza tofauti zao kwa njia ya kidiplomasia.
Mjumbe huyo alikutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na Rais Paul Kagame.
Miongoni mwa wanyarwanda waliokimbilia Afrika ya
kusini ni Generali Kayumba Nyamwasa ambaye amekuwa akilaumu utawala wa
Rwanda kwa kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi yake ambayo
amenusurika.
Kwa upande mwingine Serikali ya Rwanda inakanusha vikali kuhusika na tuhuma hizo.
Kayumba Nyamwasa anajulikana kama mtu
aliyetangaza wazi kupiga vita utawala wa Rwanda na anatuhumiwa kuhusika
katika mashambulizi ya hapa na pale yanayogharimu maisha ya watu na
mali.
0 comments:
Chapisha Maoni