Rais wa mpito wa Ukraine, Olexander Turchynov, ameonya kuhusu
tisho la kusambatarika kwa nchi hiyo kufuatia kuondolewa mamlakani kwa
aliyekuwa Rais, Viktor Yanukovych.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo upinzani ukitokota katika maeneo
ya Ukraine ambapo Kirusi kinazungumzwa dhidi ya serikali ya mpito.
Bunge la Ukraine limechelewa kuiunda serikali ya mseto.
Tangazo lilitarajiwa siku ya Jumanne kufuatia kung’atuliwa mamlakani
aliyekuwa Rais Viktor Yanukovych, lakini Rais wa mpito Olexander
Turchynov, amesema kuwa litatolewa siku ya Alhamisi ili kuruhusu
mashauriano kuendelea.
Turchynov ameelezea wasiwasi wake kwa kile alichokitaja kama hatari ya kugawanyika kwa baadhi ya maeneo nchini Ukraine.
Kumetolewa waranti ya kukamatwa Yanukovych kwa madai ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji, lakini hajulikani aliko.
Wanadiplomasia wakuu wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika mji mkuu
Kiev kujadili usaidizi wa kifedha kwa serikali ya mpito, huku nchi hiyo
ikitishiwa na mdororo wa kiuchumi kufuatia maandamano ya miezi mitatu.
Kumekuwa na wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa kuwa huenda Ukraine
ikagawanyika mara mbili; upande mmoja ukiwa karibu na Umoja wa Ulaya, na
mwingine ukiegemea upande wa Urusi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague, anasafiri kwenda Washington- Marekani, kulijadili suala hili.
Katika taarifa aliyoitoa bungeni, alisema kuwa Ukraine inahitaji
msaada wa dharura wa fedha wa kimataifa ili kuimarisha uchumi wake
unaozorota.
Ingawa kumekuwa na msimamo mkali kutoka kwa Urusi, Hague, amesema
kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Umoja wa Ulaya na Urusi kufanya kazi
pamoja.
Hague alisema, ‘Azimio letu kuu ni kuendeleza demokrasia, kutetea haki za kibinaadam, na kufuatwa kwa sheria nchini Ukraine.
Hii sio kuhusu uamuzi wa Ukraine kuchagua kati ya Umoja wa Ulaya ama
Urusi. Ni kuhusu kuielekeza nchi hiyo katika njia ya kidemokrasia katika
siku zijazo’.
0 comments:
Chapisha Maoni