Jumatano, Januari 20, 2016

WANAWAKE MAREKANI WAUNGA MKONO WENZAO WAISLAMU

Mamia ya wanawake wa mji wa San Diego katika jimbo la California nchini Marekani wamekusanyika katika Bustani ya Balboa na kutangaza mshikamano wao na wanawake Waislamu wa mji huo.
Ripoti zinasema karibu wanawake 400 wasio Waislamu wa San Diego walikusanyika katika Bustani ya Balboa wakiwa wamevaa shungi na vazi la hijabu kama la wanawake wa Kiislamu kuonesha mshikamano wao na wanawake Waislamu wanaokabiliwa na ubaguzi na pengine ukatili na mashambulizi ya kimwili na kinafsi. Maandamano na mjumuiko huo ulihudhuriwa na wanawake wa jumuiya mbalimbali za mji wa San Diego ambao walitoa wito wa kulindwa wanawake wa Kiislamu kutokana na hujuma zinazowalenga katika jamii ya Marekani hususan baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika mji wa San Bernardino katika jimbo la California. Watu 14 waliuawa katika shambulizi hilo lililofanyika Disemba 2, 2015.
Mashambulizi hayo na yake ya Paris mwishoni mwa mwaka uliopita yamezidisha mashinikizo na kutumiwa vibaya na wanasiasa katika kampeni za uchaguzi wa Rais zilizopambamba moto nchini Marekani dhidi ya Waislamu hususan wanawake wanaovaa vazi la staha la hijabu.

0 comments:

Chapisha Maoni