Washukiwa 28 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuhusika na jaribio la mapinduzi yaliyofeli mwaka jana 2015 nchini Burundi huenda wakafungwa jela maisha.
Adolphe Manirakiza, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali ya Bujumbura amependekeza kuwa, washukiwa hao wahukumiwe kifungo cha maisha jela. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi nchini humo, Cyrille Ndayikure pamoja na makamanda wakuu wa jeshi na polisi ya Burundi wamekiri kuhusika katika mapinduzi hayo ambayo yalifeli mwezi Mei mwaka jana. Habari zinasema kuwa, kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Godefroid Niyombare pamoja na baadhi ya wanajeshi waliohusika katika uasi na jaribio lililofeli la kumpindua Rais Pierre Nkurunziza la tarehe 13 mwezi Mei mwaka jana, bado wako mafichoni au wamekimbilia nje ya nchi. Hata hivyo washukiwa hao wametetea uamuzi wao wa kufanya jaribio la mapinduzi ambayo yalifeli, na kusema kuwa, mapinduzi ya kijeshi yalikuwa njia pekee ya kuikwamua Burundi katika mgogoro unaoendelea nchini humo. Burundi ilitumbukia katika machafuko na ghasia za ndani baada ya Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kuwania tena urais kwa kipindi cha tatu mfululizo mwezi Aprili mwaka jana. Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo yanayofanyika mjini Arusha nchini Tanzania yanafanyika bila uwepo wa wawakilishi wa upande wa serikali.




0 comments:
Chapisha Maoni