Ijumaa, Januari 15, 2016

SERIKALI YATUMBUA JIPU LA MGODI WA MAKAA YA MAWE KYELA, MBEYA

Serikali imesimamisha shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe ya Kampuni ya Off Route Technology iliyopo Kyela ikiwemo kukamata vifaa vya uchimbaji na kuhakikisha kuwa vinakuwa chini ya uangalizi wa Mkoa wa Mbeya hadi hapo uchunguzi dhidi ya uhalali wa kampuni hiyo kuchimba makaa utakapokamilika.
Hatua hiyo inafuatia ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo kutembelea mgodini hapo na kubaini kuwa, kampuni hiyo inachimba makaa bila kuwa na leseni halali ya uchimbaji madini.
Aidha, Prof. Muhongo ameitaka kampuni hiyo kulipa kodi zote za Serikali ikiwemo inazodaiwa na Halmashuri tangu ianze kufanya shughuli za kuchimba.
Aidha, ili kujua undani wa suala hilo, Prof. Muhongo ameitisha kikao kifanyike kati ya mgodi huo , Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania ( TMAA), Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini Magharibi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyela, tarehe 18 Januari, 2016 chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.
"Hawa watu wamechimba makaa, wameuza bila kuwa na Leseni na tunawadai kodi zetu. Uongozi hakikisheni katika kikao hicho mnakuja na madai yenu,TMAA pia mje na madai yenu", ameongeza Prof. Muhongo.
Prof. Muhongo pia amezitaka pande zote kuwasilisha nyaraka muhimu kuhusu suala hilo, ili iamuliwe kwa kufuata sheria na taratibu stahili, "hakuna mtu atakayeonewa, kila upande uje na nyaraka zote na sisi wizarani huko ndani kwetu tutaulizana wenyewe kuhusu jambo hili halafu tutalitolea taarifa" ,amesema. Prof. Muhongo.
Akifafanua kuhusu suala hilo , Afisa Mfawidhi wa TMAA ,Mhandisi Jumanne Mohamed amesema kuwa, awali Wakala huo ilifanya ukaguzi na kubaini kuwa kampuni hiyo hailipi kodi na kuwa yapo malimbikizo ya madai ambayo yalipaswa kulipwa na kuongeza kuwa baada ya mawasiliano juu ya suala hilo, kampuni iliahidi kulipa kwa awamu jambo ambalo halijafanywa hadi sasa.
Kampuni ya Off Route Technology, ipo katika Kijiji cha Ngana Wilaya ya Kyela mkoa wa Mbeya.

0 comments:

Chapisha Maoni