Jumatano, Januari 20, 2016

NDALICHAKO AAGIZA KUFUTWA MFUMO WA GPA NA KURUDISHWA DIVISHENI

Serikali imeliagiza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kufanya mapitio ya mfumo unaotumika sasa wa wastani wa alama za mtihani (GPA), ili kuangalia uwezekano wa  kurejea katika mfumo wa awali wa kupanga madaraja kwa mfumo wa divisheni.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof.  Joyce Ndalichako, wakati akizungumza na waandishi wa habari .
Alisema pamoja na serikali kutoa siku saba kwa baraza hilo kutoa sababu ya kuhama kutoka mfumo wa divisheni na kwenda katika mfumo wa GPA, bado baraza hilo limekuwa likitoa maelezo zaidi kuliko sababu za kuhamia mfumo huo.
Alisema hoja ya kuwa mfumo huo ulitokana na maagizo ya serikali haina nguvu kwa kuwa tayari baraza hilo ndilo linalotakiwa  kubeba dhamana ya madaraja ya ufahulu.
Prof. Ndalichako alisema kutokana na bazara hilo kuendelea kutoa maelezo ambayo hayatoi sababu za kuhamia mfumo wa GPA, serikali imelitaka kufanya mapitio ya mfumo huo kwa lengo la kurudi katika mfumo wa awali wa divisheni.
Alisema baraza hilo linatakiwa kuweka viwango vya ufaulu kwa kuzingatia azma ya nchi kuelekea katika uchumi wa kati.
Aidha, Prof. Ndalichako aliitaka Necta  kufuta karatasi ya pili ya watahiniwa wa kujitegemea ambayo imeanzishwa kama alama ya mtihani wa muendelezo wakati kiuhalisia ni mtihani wa mwisho.
“Wizara haiwezi kufikia azma yake ya kuelekea uchumi wa kati bila kuhakikisha viwango vya ufaulu vinawezesha nchi kutoa watalaamu wenye stadi na maarifa stahiki  badala ya kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti lakini hawakidhi mahitaji katika soko la ajira,’’ alisema.
Aliongeza kusema, wizara ina amini kuwa elimu ndiyo hazina ya nchi, hivyo itasimamia zaidi ubora wa elimu na kufuatilia kwa karibu kinachoendelea  darasani ili kuhakikisha wahitimu wanakidhi matarajio na kuchangia maendeleo ya taifa.

0 comments:

Chapisha Maoni