Kiwango cha watoto wanaozaliwa barani Afrika kinaongezeka kwa kasi na jamii ya Waafrika itakuwa maradufu, kwani inakadiriwa kufikia watu bilioni moja na milioni mia mbili ifikapo mwaka 2050.
Ripoti iliyotolewa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imeeleza kuwa, kiwango cha uzaaji barani Afrika kinaongezeka kwa kasi mno na ifikapo mwaka 2050, bara la Afrika litakuwa na wakazi robo ya watu wote duniani.
Ripoti hiyo ya UNICEF imeongeza kuwa, hadi kufikia nusu ya karne ya 21 Miladia, asilimia 40 ya watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano itakuwepo barani Afrika.
Imeelezwa kuwa, Nigeria ambayo inahesabiwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, pekee itahodhi asilimia kumi ya watoto watakaozaliwa barani humo kufikia 2050. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, hadi kufikia mwaka 2030 idadi kubwa ya Waafrika wataishi mijini badala ya vijijini.
UNICEF imeeleza kuwa, zaidi ya nusu ya watoto wanaofariki dunia wanatoka barani Afrika, na katika kila watoto 11, mmoja wao hufariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.
0 comments:
Chapisha Maoni