Ijumaa, Mei 16, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kwa mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na utajiri mkubwa wa madini na alimasi, imekuwa ikizingatiwa na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi.

Siku kama ya leo miaka 512 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine ya huko America ya Kati, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake.

Siku kama ya leo, miaka 1159 iliyopita, alifariki dunia Abdullah bin Muslim Dinuri, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63. Ibn Qutayba alizaliwa mjini Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinuri, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi. Alimu huyo aliandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni pamoja na “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Ghariibul-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.”

Na siku kama ya leo miaka 896 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Abu Mansur Muhammad bin Abdul-Malik, maarufu kwa jina la Ibn Khayrun, mtaalamu wa hadithi na ustadhi katika elimu ya qiraa yaani kisomo cha Qur’ani. Kuna vitabu kadhaa kutoka kwa Ibn Khayrun vikiwemo vya “Al-Miftaah” na “Al-Maudhuu.”

0 comments:

Chapisha Maoni