Jumatano, Januari 08, 2014

BAADA YA WEMA SEPETU KUPEWA 'NOTICE' YA KUHAMA KATIKA NYUMBA ANAYOISHI...SASA DIAMOND KUMNUNULIA NYUMBA YA TSH.125 MILIONI

Nasibu Abdul ‘Diamond’ anadaiwa yuko kwenye mchakato wa kumnunulia jumba la kifahari mpenzi wake wa ‘nenda rudi’, Wema Sepetu, Amani limeinyaka hii.
Nasibu Abdul ‘Diamond’
Kwa mujibu wa chanzo, Diamond ameamua kuingia kwenye kujikamua huko kufuatia taarifa kwamba, mmiliki wa nyumba anayoishi Wema kwa sasa (jina lipo), Kijitonyama, Dar es Salaam amemwamuru mlimbwende huyo kuhama kwenye mjengo wake mara baada ya kumaliza mkataba mwezi Juni, mwaka huu. Awali mjengo huo aliutangaza ni wake.
Wema Sepetu
“Mwenye nyumba anayoishi Wema kwa sasa amekataa mrembo huyo kuendelea kuishi pale, akimaliza mkataba wake Juni, mwaka huu basi, hataki tena. 
“Sasa Diamond aliposikia hilo akamwambia Wema isiwe tabu, akamuahidi kumnunulia nyumba ya kifahari yenye thamani ya shilingi milioni mia moja na ishirini na tano.
“Nadhani hiyo nyumba ipo tayari, ndiyo maana amemtajia na bei. Lakini ninavyojua mimi ipo Mwananyamala,” kilisema chanzo.
Kuhusu nyumba ya sasa, ni kweli ‘kifo cha nyani miti yote huteleza’ kwani Wema anatakiwa kutoendelea na mkataba mpya ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama ya Ilala, Dar es Salaam kuamuru anyang’anywe lile gari lake la kifahari aina ya Audi Q7 lenye usajili wa T 973 BUJ na kukabidhiwa mmiliki wake halali, Shadrack Tweve. 
Wema alipewa gari hilo na mwanaume anayedaiwa ni mpenzi wake anayejulikana kwa jina la Clement ambaye alilikopa kwa mmiliki huyo lakini alikuwa akikwepa kulipa deni la shilingi milioni 90.
Akizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar, mmoja wa ‘kruu’ ya Wema ambaye hakutaka jina lake lionekane gazetini alisema kwa sasa Wema yuko katika kipindi kigumu baada ya kumwagana na kigogo huyo aliyekuwa akidaiwa kumpa jeuri na kufuatia kuamriwa kuhama kwenye nyumba hiyo.
Chanzo chetu kikazidi kumwaga data kuwa mbali na Wema kuachana na Clement, bado mrembo huyo amekuwa katika kipindi kibaya zaidi baada ya kunyang’anywa gari hilo ambalo ndilo alilokuwa akilitumia.

0 comments:

Chapisha Maoni