Ijumaa, Agosti 02, 2013

MILA , DESTURI NA TAMADUNI NDICHO CHANZO KIKUBWA CHA MAAMBUKIZI NJOMBE

Mila, desturi na tamaduni ni miongoni mwa mambo mengi yanayoenziwa na hata kuheshimiwa duniani ikiwamo Tanzania.

Linda Chatilla, Ofisa afya, Mkoa wa Njombe 
Kutokana na umuhimu wake kila jamii imekuwa ikihakikisha inazienzi na kuzitunza tamaduni zake na kurithisha vizazi vinavyokuja.Kutokana na umuhimu wake, haishangazi kuona wakazi wa Mkoa mpya wa Njombe nao wakiwa wanaenzi, kutunza na kurithishana tamaduni zao kwa watoto wao.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea, tafiti zinaonyesha kuwa utamaduni wa asili wa wakazi hao wa kucheza ngoma za asili ni miongoni mwa mambo yanachochea ongezeko la maambukizi ya Ukimwi, hali inayoufanya mkoa huo kukamata namba moja kwa idadi ya walioathirika nchini.
Tamaduni zinazoenziwa na wakazi wake ni pamoja na ngoma za asili kama Mnanda, Kiholda na Matuli ambazo huandaliwa kwa muda mrefu na kukutanisha watu wa rika mbalimbali.
Mbali na ngoma za asili, ulevi kupindukia wa pombe za kienyeji, kurithi wajane, mwingiliano wa watu katika shughuli za kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kupandisha kasi ya maambukizi ya Ukimwi katika mkoa huo.
Haya yamebainika katika utafiti uliotolewa na taasisi ya HIV, Malaria Indicators Survey ya mwaka 2011/12.
Wakazi wa Njombe ambao ni wa makabila ya Wabena, Wakinga, Wamanda Wapangwa, na Wakisi wanazo mila, tamaduni na desturi zao ambazo zinatajwa kuchangia ongezeko la maambukizi ya Ukimwi.
Ngoma hizo ni maarufu, zinaheshimiwa na wakazi wa mkoa huo na huchezwa katika matukio mbalimbali, lakini huwa maarufu zaidi katika baadhi ya vijiji vya Ludewa na Makete.
Wakazi wa mkoa huu hutumia (pombe) kinywaji cha kienyeji cha ulanzi, ambacho hutengenezwa kutoka katika miti ya mianzi. Pombe hii hunywewa na watu wa rika zote. Mbali na ulanzi, vilevile kuna komoni na kimpumu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mila, desturi na tamaduni hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya maambukizi ya Ukimwi.
“Tamaduni hizi zote zikiwemo ngoma za kienyeji, unywaji wa pombe zina mchango mkubwa katika kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya Ukimwi, hivyo iko haja kwa timu ya afya ya mkoa kutoa ushauri kwa viongozi wa afya wa halmashauri namna ya kuepuka ugonjwa huo.

0 comments:

Chapisha Maoni