WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema
Serikali kwa sasa imeanza kusambaza kompyuta katika vyuo vikuu nchini
kwa lengo la kuboresha elimu kwa wanafunzi. Pia, amesema baadaye
Serikali itaanza kusambaza kompyuta ndogo zinazobeba vitabu kidijitali,
maarufu kama tabuleti (tablets) kwa wanafunzi.
Alisema hayo bungeni jana wakati wa
kipindi cha maswali ya papo kwa hapo. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalumu, Maryam Msabaha (Chadema).
Nchi zilizoendelea zimewekeza sana katika elimu, lakini sisi Tanzania kwa nini hatuwekezi katika elimu?
Alihoji.
Sisi hapa mtoto akienda shule asubuhi anabeba fagio, lakini kwa wenzetu anabeba kompyuta. Hata kwa majirani zetu Kenya, mtoto anabeba lap top asubuhi.
Msabaha aliongeza
Je huoni kwamba wakati umefika sasa kwa wanafunzi wetu wa darasa la Kwanza hadi la Saba wawe na lap top?
Akijibu swali hilo, Pinda alisema Serikali imejitahidi
kuboresha Sekta ya Elimu nchini, kuanzia shule za msingi, sekondari,
vyuo na vyuo vikuu.
Waziri Mkuu alisema inachofanya Serikali
kwa sasa ni kutatua matatizo hayo ya msingi katika Sekta ya Elimu hatua
kwa hatua. Kuhusu suala la kusambaza kompyuta shuleni na vyuoni, Waziri
Mkuu alisema kwa sasa lengo la Serikali ni kusambaza kompyuta katika
vyuo vikuu na baada ya hapo ndipo zitafuata shule za sekondari na
msingi.
Waziri Mkuu alisema Serikali ingependa
wanafunzi wawe na tabuleti na lap top, lakini uwezo wa Serikali ni mdogo
na ndiyo maana wameamua kuanza na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Waziri Mkuu aliulizwa swali lingine na
Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema), ambaye alitaka kujua ni
lini atawarejesha madarakani madiwani watatu wa Jimbo la Ilemela Mkoa wa
Mwanza, waliofukuzwa na Meya wa Manispaa hiyo.
Meya wa Ilemela alifukuza madiwani watatu wa Chadema, kwa madai hawakushiriki vikao vitatu vya Baraza la Madiwani. Nilikuletea vielelezo na wewe ulifanya uamuzi wa kuwarejesha, lakini nasikia ulipata pingamizi kutoka Mkoa wa Mwanza. Sasa ni mwaka mmoja na miezi sita tangu wamefukuzwa. Je, ni lini utawarejesha?
Alihoji Kiwia.
Waziri Mkuu alisema hakuna kitu chochote cha makusudi kinachochelewesha kutoa uamuzi wa mwisho wa suala hilo.
Alisema ni kweli alishafanya uamuzi wa
kuwarejesha, lakini alipata pingamizi (counter request) kwamba maelezo
aliyopewa hayakuwa sahihi.
Alisema baada ya hapo, alirejesha tena
suala hilo kwa wataalamu na mamlaka zingine ili wamshauri tena na kwamba
ni juzi tu amepata mapendekezo ya wataalamu hao na mamlaka hizo. Pinda
alimtaka Mbunge huyo kuwa na subira, kwani uamuzi atautoa hivi karibuni.
Tarehe siwezi kusema ni lini. Lakini suala hili nitalipa umuhimu mkubwa. Nitafanya uamuzi hivi karibuni na nitarejesha uamuzi huo mkoani Mwanza,
alisisitiza.
Waziri Mkuu ndiye mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
0 comments:
Chapisha Maoni